Media centre

Press releases

Speeches

Feature stories

 

21 Oktoba 2013: Kutoka Shirika la UNICEF juu ya Siku ya Unawaji Mikono Duniani : Suluhisho rahisi ufumbuzi rahisi kwa manufaa makubwa – Uwezo uko Mikononi Mwetu

Dar es Salaam , Oktoba 21, 2013 – Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) linaungana na mamia kwa maelfu ya watu nchini Tanzania leo katika kuadhimisha mwaka wa sita wa siku ya ya Unawaji Mikono Duniani, na kusisitiza umuhimu wa kunawa mikono kwa sabuni kama njia madhubuti , rahisi na nafuu kwa kuzuia magonjwa ya kuhara.

"Kitendo rahisi cha kunawa mikono kwa sabuni ni moja ya njia bora ya kuokoa maisha ya watoto, " anasema Kiwe Sebunya, Mkuu wa Kitengo cha Programu ya Maji, Afya na Usafi wa Mazingira wa Shirika la UNICEF nchini Tanzania. " Kunawa mikono kabla ya kula na baada ya kutoka chooni hupunguza kuenea kwa magonjwa ya kuhara na manufaa yake ni ya muda mrefu kwa afya na ustawi wa watoto na jamii kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Shirika la UNICEF na Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii , kuhara bado ni miongoni mwa magonjwa makuu matano yanayochangia katika vifo kwa watoto wadogo wenye umri chini ya miaka mitano nchini Tanzania. Takwimu zinaonyesha kwamba moja ya tatu ya vifo vya watoto kutokea ndani ya mwezi wa kwanza wa maisha ya watoto vinatokana na maambukizi au magonjwa ya kuhara yanayosababishwa na ukosefu wa maji safi na salama, mazingira machafu na kutozingatia tabia za usafi. Madhara mengine yatokanayo na ukosefu wa maji safi na salama, mazingira machafu na kutozingatia tabia za usafi ni kudumaa (mtoto kuwa na kimo kifupi kisichoendana na umri na kuathiri ukuaji). Takwimu zinaonyesha kwamba zaidi ya asilimia 40 ya watoto chini ya miaka mitano nchini Tanzania wamedumaa.

Kunawa mikono kwa sabuni ni mojawapo ya njia rahisi na yenye gharama nafuu kuzuia maambukizi. Takwimu za utafiti wa afya ya uzazi na mtoto za mwaka 2010 nchini Tanzania zinaonyesha kwamba ni mtu mmoja tu kati ya watano ambaye ananawa mikono kwa sabuni kabla ya kuandaa chakula; na mtu mmoja kati ya watanzania wawili hapati huduma ya maji safi na salama. Aidha , kiwango cha matumizi ya vyoo bora ni asilimia 22 kwa mjini na asilimia 9 kwa vijijini. 

Maadhimisho ya siku ya kunawa mikono duniani kwa Tanzania husaidia kuhamasisha umuhimu wa kunawa mikono kwa sabuni na kukuza uelewa wa namna inavyosaidia katika kuokoa maisha ya watoto na jamii kwa ujumla.

Karibu watu milioni 3 ( ikiwa ni pamoja na wanafunzi wa shule za msingi) watashiriki katika maadhimisho haya kwa kupitia washa na zoezi la kunawa mikono. 

Maadhimisho haya yalizinduliwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii , UNICEF na mashirika mengine katika Shule ya Msingi Mugulani, wilaya ya Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam. Shughuli zilizoambatana na uzinduzi huu ni pamoja na michezo ya kuigiza, zoezi la kuawa mikono kwa kuhusisha watu wengi, usambazaji wa ujumbe kupitia vipeperushi na mabango unaohamasisha kunawa mikono nyakati tano muhimu ambazo ni; kabla ya kutayarisha chakula, kabla ya kula, kabla ya kumlisha mtoto, baada ya kutoka chooni, na baada ya kumsafisha mtoto aliyejisaidia.

Aidha, maadhimisho hayo yameambatana na uzinduzi wa msafara wa sabuni amabao utatembelea mikoa nane ya Tanzania bara ukipitia kwenye jumla ya shule 24 kwa kipindi cha majuma matano kuanzia leo. Msafara huu unalenga kuhamasisha unawaji mikono kwa sabuni, njia sahihi za kutibu na kutunza maji ya kunywa majumabani, na matumizi ya vyoo bora. Hii itafanyika kupitia nyimbo, ngonjera, mashairi, michezo ya kuigiza, mashindano ya usafi, na kugawa vipeperushi. 

Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya kunawa mikono duniani mwaka huu ilitangazwa na Ushirikiano wa Kimataifa wa taasisi za umma na binafsi, ambapo shirika la UNICEF ni mshirika, inasema “Uwezo uko mikononi mwako”, kwa sababu, ushirikiano huu unaamini kwamba kila mtu ana uwezo wa kujenga jamii yenye afya kupitia unawaji mikono kwa sabuni. Hata hivyo , Tanzania imeandaa kauli mbiu yake ambayo inaendana na kauli mbiu ya kimataifa. Kauli mbiu hii ni Usafi nai ustaarabu , unaanza na sisi ; tumia choo bora, nawa mikono kwa sabuni , okoa maisha ya watoto. Ushahidi uko wazi , hivyo kila mtu-mama mtoto, mwalimu, na mwanajamii ana fursa ya kuchangia kuboresha afya ya watu kwa kunawa mikono kwa sabuni "anaongeza Kiwe Sebunya. " Kama ungejua kitu kikubwa ambacho kingeweza kufaidisha dunia, ungekifanya. Kila mmoja wetu ana uwezo huo- basi loanisha mikono, paka sabuni, sugua itoe povu na suuza kwa maji.

 

 
Search:

 Email this article

unite for children